8 Septemba 2021 - 12:29
Umoja wa Mataifa: Huduma muhimu nchini Afghanistan zimo katika hali ya kusambaratika

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya uratibu wa misaada ya kibinadamu, (OCHA) imetangaza kuwa, mamilioni ya wananchi wa Afghanistan wanahitajia misaada ya chakula pamoja na huduma za kiafya.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Taarifa ya Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya uratibu wa misaada ya kibinadamu, (OCHA), imebainisha  kwamba, kwa sasa sekta ya utoaji huduma nchini Afghanistan inakabiliwa na hali mbaya na imo katika hatua ya kusambaratika.

Asasi hiyo iliyoko chini ya Umoja wa Mataifa imezitaka nchi wahisani kutoa misaada zaidi katika mkutano ujao wa Septemba 13 wenye lengo la kukusanya misaada kwa ajili ya nchi hiyo. 

Umoja wa Mataifa umesema, kwa sasa kunahitajika kiasi cha dola milioni 200 za haraka kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa Afghanistan ambao wanakabiliwa na matatizo mbalimbali ukiwemo uhaba wa chakula na ukosefu wa huduma nyingine muhimu kama za afya na matibabu.

Hivi karibuni Umoja wa Mataifa ulitahadharisha kuhusiana na uhaba mkubwa chakula nchini Afghanistan na kutoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka za kuisaidia nchi hiyo.

Ramiz Alakbarov, mratibu wa kieneo wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan amesema kuwa, theluthi moja ya wakazi milioni 38 nchini humo wanakabiliwa na hali ya dharura au mgogoro wa usalama wa chakula.

Jumapili tarehe 15 mwezi uliopita wa Agosti serikali ya Rais Muhammad Ashraf Ghani ilisambaratika na kiongozi huyo kuikimbia nchi baada ya Taliban kuingia Kabul mji mkuu wa Afghanistan. Wachambuzi wa mambo wanasema, hatua ya Taliban ya kuudhibiti mji wa Kabul imehitimisha uvamizi wa miaka 20 wa Marekani na nchi nyingine za Magharibi kwa kisingizio cha kuijenga upya Afghanistan.


342/